Ijumaa, 29 Mei 2015

MISHAHARA YA WALIMU KUONGEZWA AGOSTI

87df3-jkNa ,Arusha.
Raisi Jakaya Kikwete amesema kuwa walimu watarajie nyongeza ya mishahara itakayoanza mwezi Agosti mwaka huu ikiwa ni moja kati ya jitihada za serikali katika kuboresha maslahi ya walimu nchini.

Kikwete akihutubia Mkutano Mkuu wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT ) uliofanyika jijini Arusha jana amesema kuwa nyongeza hiyo itahusisha walimu wote wanaolipwa kima cha chini  cha mshahara na kima cha juu pasipo kutaja kiwango kilichoongezeka.

“Wakati mnachukua mishahara yenu benki mwezi Agosti mtaona tofauti ambayo ni nyongeza ya msahara ,wenzenu wa chama cha Wafanyakazi waliniomba nisitangaze  niongeze kimya kimya ili wafanyabiashara wasipandishe bei ya bidhaa” Alisema Raisi Kikwete

Aidha Raisi Kikwete alisema kuwa serikali inaendelea na jitihada za kuhakikisha kuwa inaboresha elimu nchini ikiwa ni pamoja na kuboresha maslahi ya walimu nchini,kuongeza vifaa vya kujifunzia na kufundishia,nyumba za walimu,vitabu  na maabara.

Amesema kuwa madai ya walimu wanayoidai serikali yatalipwa kwa awamu iwapo uhakiki utakamilika kwa sasa wanatarajia kulipa kiasi cha shilingi bilioni 7 kwa walimu 70100 watalipwa Agosti mwaka huu.

“Katika kufanya uhakiki wa madai ya walimu ikiwemo malimbikizo ya mishara,posho za kufundishia,uhamisho tuligundua kuwa wako baadhi ya watu walifanya udanganyifu lakini sasa tunamalizia kufanya uhakiki ili fedha hizo zilipwe” Alisema Kikwete

Katibu Mkuu wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT) Alhaji Yahaya Msulya amemtaka Raisi Kikwete kushughulikia suala la posho ya kufundishia kwa walimu kwani walimu ni kundi linalofanya kazi kwa muda mrefu kuliko watumishi wengine wa serikali.

“Mwalimu anaingia shuleni saa 1:30 asubuhi anatoka saa 3:00 mda huo anatakiwa kusahihisha kazi za wanafunzi na kuandaa masomo ya kufundisha kesho hivyo anatumia muda mwingi sana katika kazi ni vyema serikali ikaliangalia suala hili” Alisema Katibu huyo

Katibu huyo ameupongeza uamuzi wa serikali kutoa bure elimu ya msingi na sekondari ambao utawasaidia watoto wengi hasa waliotoka kwenye familia zenye kipato cha chini.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni