WAZIRI
MKUU Mizengo Pinda amewataka Watanzania wote nchini wajenge tabia ya
kuandika wosia ili kuondoa matatizo ya mirathi pindi mume anapoaga
dunia.
Ametoa
wito huo leo mchana (Ijumaa, Mei 29, 2015) wakati akizindua kampeni ya
kuandika wosia kwenye maadhimisho ya miaka 25 ya Chama cha Wanasheria
Wanawake Tanzania (TAWLA) yaliyofanyika katika viwanja vya Karimjee,
jijini Dar es Salaam.
Akizungumza
mara baada ya kushuhudia uandishi wa wosia mbele ya wakili, Waziri Mkuu
alisema uandishi wa wosia ni suluhisho la migogoro mingi
inayosababishwa na wanandigu ambao wakati mwingine wala hawakushiriki
kuchuma mali wanayogombea.
“Kuandika
wosia siyo uchuro kama ambavyo watu wengi wanadhani… ninatoa kwa
Watanzania kuandoak wosia mapema kwani inasaidia kuondoa matatizo ya
mirathi baada ya mmoja wao kuondoka duniani,” alisema.
“Mtua
anapaswa kutamka mali nilizonazo ni kadhaa na endapo nitakufa mali hii
apewe fulani, na hii fulani na nyingine fulani. Hati hii inapaswa
kutunzwa kwa mwanasheria, benki au kwa Kabidhi Wasii. Tusipolifanya
hili, matatizo yataendelea kuwakumba wajane na watoto walioachwa na
marehemu,” alisema.
Aliipongeza
TAWLA kwa kuchukua jukumu la kuhamasisha umma kuhusu suala la uandishi
wa wosia lakini pia akawataka wanachama wa TAWLA wajikite zaidi kwenye
kutetea haki za makundi maalum kama walemavu wa ngozi, vikongwe na watu
kutoka makabila madogodogo. “Haya makundi yana shida zao ambazo
hazifanani na watu wengine. Nendeni vijijini, mkatoe elimu, jueni
changamoto wanazokabiliana nazo, wasikilizeni shida zao na muone ni njia
gani mnaweza kuwasaidia,” alisema.
Akitoa
mfano, Waziri Mkuu alisema katika kipindi cha miaka nane kuanzia mwaka
2006 hadi 2014, jumla ya vikongwe 2,219 waliuawa katika mikoa ya Geita,
Simiyu, Mara, Kagera na Mwanza ambayo alisema yote iko Kanda ya Ziwa.
“Mauaji haya yanasababishwa na imani
potofu za kishirikina; jamii kuwa na uelewa mdogo wa sheria; ukosefu wa
imani za kiroho; ukosefu wa elimu; na waganga wa kienyeji kupiga
ramli,” alisema.
Alisema
makabila madogo yanakabiliwa na matatizo ya ardhi ambayo ndiyo tegemeo
lao kuu, vikongwe na watu wenye ulemavu wa ngozi wanatishiwa usalama wa
maisha yao bila sababu yoyote. “Nendeni mkatoe elimu zaidi kwa watu hawa
ili tuwalinde wazee wetu, makabila madogo kama Wahadzabe na Wasandawe
pamoja na ndugu zetu wenye ulemavu wa ngozi,” alisisitiza.
Mapema,
akimkaribisha Waziri Mkuu kuzungumza na washiriki maadhimisho hayo,
Mwenyekiti wa TAWLA, Bi. Aisha Bade alisema chama hicho kimetumia
wanasheria wanawake zaidi ya 200 na wasaidizi wa kisheria 400
(paralegals) kutoa msaada wa kisheria kwa watu mbalimbali ambao hawana
uwezo kumudu gharama za kesi.
“Katika
mwaka 2014, tumetoa msaada wa kisheria kwa watu zaidi ya 10,000 ambao
hawana uwezo kumudu gharama za kesi kwenye mikoa mbalimbali hapa
nchini,” aliongeza.
Naye
Balozi wa Sweden nchini, Bw. Lennarth Hjelmaker, akizungumza kwa niaba
ya wadau wa maendeleo nchini alisema Serikali ya nchi hiyo ilitenga
kiasi cha sh. bilioni 4 kusaidia mpango wa miaka minne wa chama hicho wa
kuimarisha utawala bora, uwajibikaji na usawa wa kijinsia.
“Hadi
sasa tumekwishatoa sh. bilioni 3.5 ambazo kati ya hizo, sh. bilioni 1.1
zimetumika kusaidia wanawake wapatiwe haki zao; sh. milioni 500
zimetumika kutoa mafunzo kwa watumishi wa afya ili watoe huduma rafiki
za afya ya uzazi kwa vijana na sh. milioni 700 zimetumika kutoa mafunzo
kwa viongozi wa ngazi ya chini wanaohusika kutoa maamuzi. Kiasi cha sh.
bilioni 1.2 kimetumika kuendeleza shughuli za chama,” alifafanua.
Pamoja
na kutoa elimu kwa jamii na kutetea haki za akinamama na wasichana,
Balozi huyo wa Sweden alisema kuna haja ya kuweka mkazo ili kuwafikia
wanaume na wavulana wengi zaidi ili waweze kujirekebisha na kubadili
tabia na mitazamo yao dhidi ya wanawake na wasichana.
IMETOLEWA NA
OFISI YA WAZIRI MKUU,
2 MTAA WA MAGOGONI,
S. L. P. 3021,
11410 DAR ES SALAAM
IJUMAA, MEI 29, 2015.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni